Mdhihirisho wa Lango la Masihi
__largepreview__.webp)
Download the English Version: The Manifestation of the Gate of the Messiah - 2026 Prophetic Utterances
"Umeingia katika majira ya matendo ya Masihi katika maisha yako, wewe utakuwa Lango la Masihi."
Ezekieli 44:2-3; Yohana 10:7-10
Matamko ya Kiunabii na Bishop Dr. Manasse DM
Mwaka huu kutakuwa na roho inayodhihirika sana, roho ya waamaleki na washirika wao, wamidiani. Dhumuni lao ni kumwinua mwanadamu ili apate kupambana na kila kilicho kusudi la Mungu duniani. Hata hivyo, Mungu anaenda kudhihirisha Lango la Masihi kuwa wazi ili Mungu amwinue mwanadamu atakayehakikisha ya kwamba kumefutwa kila namna ya agenda ya shetani duniani.
Na kwa sura hiyo, 2026, kuna Mdhihirisho wa Lango la Masihi. Masihi mwenyewe ni jambo jingine tofauti, na Lango lake kutenda kazi ni jambo jingine tofauti. Yeye hana mwingiliano wowote na kiumbe yoyote, lakini wewe utakuwa Lango la Masihi.
Nikatazama, nami nikaona katika roho, jeshi lenye nguvu, jeshi linalotembea katika namna ya kushangaza—na jeshi hili ni la watumishi katika kizazi chetu ambao ni warithi wa mababa waliotangulia. Hawakuwa wengi, hawakuzidi kumi. Nao walikuwa wanatembea kwa pamoja kama jeshi la farasi, na mawimbi ya damu yalikuwa yanatembea pamoja na wao, na nyuma yao kulikuwa na mawimbi ya moto yanayoambatana nao.
Nami nikatazama kwa umakini wote, nikaogopa, nikitafakari kilichokuwa kinaendelea katika maisha ya watumishi hawa wa Mungu. Bwana akasema, “Hiki ndicho kizazi kinachoandaa jukwaa kwa ajili ya Mdhihirisho wa Masihi duniani katika nyakati hizi. Hili ni Lango ambalo haliwahusu wao, lakini wao wanatengeneza jukwaa kwa ajili ya Mdhihirisho wa Masihi duniani.”
Nami nikiwa natazama namna ambavyo wanaenda wakiwa na nguvu, wakiwa wanasukumwa na mawimbi ya damu mbele yao, na mawimbi ya moto nyuma yao, kwa macho yangu nikamwona Masihi kama anavyoelezwa katika kitabu cha Ufunuo 19: akiwa ameshika fimbo mkononi badala ya upanga. Nami nilipomwona, moyo wangu ukayeyuka kwa hofu kwamba amekuja kumaliza kila kitu duniani. Hapo ndipo Bwana akaanza kunena nami kuhusiana na yale yanayohusisha mwaka huu.
Bwana akasema, “Hawa watafanya mbingu ziwe wazi. Mbingu zitakuwa wazi ili malaika wa Bwana waingilie kati katika kuwasaidia. Malaika hao wa Bwana walio walinzi na wangojezi watawasaidia wateule wa Mungu wale wote walio tayari, wale wote walio na utashi. Watawasaidia kuwa aina ya watu hodari duniani, watakuwa mashujaa duniani. Watu ambao wataporomosha kabisa kazi ya yule mpinga Kristo anayeinuka ili apingane na Mungu. Tayari Mungu ana watu ambao katika hao wanaandaa mbingu ziwe wazi kwa ajili ya hao.
Dhumuni na Matendo ya Mashujaa hawa:
- Wataandaa ngome na vituo vya kiutume. Ngome zenye mamlaka ya kiutume ambazo katika hizi zitaachilia watu wenye nguvu kote kote usoni pa nchi bila kujali jinsia zao na uwezo wao. Yale wanayoyatenda, mbingu zitaambatana nao.
- Watafichua ngome za kimaeneo. Kama zilivyokuwa katika siku za Modekai na Hamani, hawa watakuwa watu wa joho la Modekai. Hamani atakuwa ametaabisha nchi kwa muda mrefu, amekaa mahala asipostahili kuwako kwa muda mrefu. Lakini hawa watakuja kudhihirisha na kufichua kila kitu ambacho ni nguvu ya Hamani na kila namna ya nguvu ya uanadamu ule wa namna ya Hamani, itaporomoka. Haya yanatokea mwaka huu! Haya yanaanza leo hii! Haya yanatokea mwaka huu! Haya yanaanza leo hii! Na wewe uwe miongoni mwa wale ambao Bwana anawaandaa.
- Bwana anawapa uwezo wa kuwaelekeza jinsi ya kufanya vita wale waliokuwa wanyonge na duni kabisa, nao watakuwa hodari na wenye nguvu usoni pa nchi. Mtu na aseme, “Na niwe mmoja wao, na niwe mmoja wao, na niwe mmoja wao, na niwe mmoja wao, na niwe mmoja wao, na niwe mmoja wao, katika jina la Yesu.”
"Haya yanatokea mwaka huu. Haya yanaanza leo hii. Na wewe uwe miongoni mwa wale ambao Bwana anawaandaa."
Mdhihirisho wa Lango la Masihi si kwa lengo la kukuchukua kwenda mbinguni au kukurejesha Yerusalemu, ni kufunguka kiunabii kuhakikisha ya kwamba msaada wa mbingu unakufikia pale ulipo. Msaada wa mbingu unakuondolea harakati za yule mwovu. Kwa upande wa pili, mwanadamu yule anayeinua kiburi chake ili akae mahala pa Kiti cha Enzi cha Mungu atainuka kwa nguvu kubwa naye ana mawe ya nguzo zake anazozitumia:
- Nguzo ya roho ya kiudini inayochanganya uchawi ndani yake
- Nguzo ya ufukara uliokithiri unaofanya watu wauze nafsi zao kwa mwovu ili tu kupata mlo mezani
- Nguzo ya wajumbe wa mauti wanaomeza uhai wa watu kupitia nguvu na shurti za miungu wa kigeni
- Nguzo ya lewiathani, joka azongazongae aliye na ngome yake katika vilindi vya maji
Hata hivyo, wale wanaobeba mafuta ya Masihi katika maisha yao wataziporomosha. Masihi anapodhihirika, watapewa majawabu ya kiuchumi yatakayofanya watu wawe na roho ya akili timamu. Masihi mwenyewe atadhihirika atetee Kiti Chake za Enzi kila mahala chini ya mbingu.
Walioko Nyuani mwa Mungu: Kuna watu ambao Mungu anawaita watu wa kundi la Daudi, Yonathani na Sauli.
- Kina Daudi ni watu wanaoenda kubeba mafuta ya Mdhihirisho wa Lango la Masihi. Hawa ni watu walio tayari kulipa gharama, watu ambao kujitoa kwao mbele za Mungu ni zaidi ya mwanadamu awezavyo kufikiri, watu walio tayari kupoteza uhai wao ili wengine wawe salama. Watu wa namna hii Mungu anawainua na mahala alipowapatia, hakuna atakayewaondoa.
- Kina Yonathani ni watu walio wema, watu ambao Mungu ana agenda nao. Lakini watu wa kundi la Yonathani wana mapungufu. Wanampenda Daudi, wana agano na Daudi, lakini hawataki kuachana na Sauli kwa kuwa Sauli ni ndugu yao, ana pesa, yuko mahala pa kiti cha enzi, ana dini, anaonekana pembe zake zinatosha kumtawanya yeyote. Daudi ana agenda na mafuta ya Mungu, lakini hana kitu, bado yuko mapangoni, na kina Yonathani hawako tayari kumfuata Daudi. Kwa sababu ya kuwa na hofu ya kumfuata Daudi, wanaendelea kuambatana na Sauli huku wakiwa wanampenda Daudi na kumsaidia ili afanikiwe. Akina Yonathani siku zote huwa wanapoteza. Mnaweza kuwa nao katika kusanyiko, familia na maeneo mengine mengi, lakini miisho yao huwa hawafiki mahala pa viti vyao vya enzi kwa sababu hawawezi kuchagua. Wanamjua mwenye mafuta na agenda ya Mungu, wanamfuata nusu; na wanamfuata yule aliye na chochote.
- Kina Sauli hapo kwanza walikuwa na Mungu, lakini Mungu amewaacha, ameondoka kwao na mawimbi ya Mungu yameenda kwenye kiwango kingine. Lakini kwa sababu ya sauti waliokuwa nayo tangu zamani, watu wameendelea kufuata kile ambacho ni alama za majivu wakati moto ukiwa haupo. Kina Sauli wataendelea kuwa na sauti ya kujaribu kuwaelekeza watu, maana hata mfalme Sauli alikaa kwenye kiti cha enzi miaka thelathini na minane zaidi Mungu akiwa amemkataa. Wanaweza kuwa mahala pa viti vya enzi, lakini Mungu hawatambui. Wanaweza kuwa na fedha, majeshi, uchawi na haya na yale, lakini tazama Mungu yuko wapi.
Kama wewe ni Daudi, huna haja ya kupambana na awaye yote, ifuate agenda ya Mungu. Kama wewe ni Yonathani, huna haja ya kukaa njia panda, itazame agenda ya Mungu ilipo na iandame kwa moyo wako wote. Iandame kwa moyo wako wote! Kama wewe ni Sauli, tazama Mungu yuko wapi katika maisha yako. Tazama Mungu yuko wapi!
Matukio Yanayotazamiwa
Ni nini basi kinatazamiwa katika mwaka huu?
- Huu ni mwaka wa Mdhihirisho wa Lango la Masihi na majira ya matendo ya Masihi mwenyewe katika maisha yako. Utakuwa ni mwaka wa kufichua hila ya Hamani na kuinua haki ya Modekai. Utakuwa ni mwaka wa kuwasilishwa pumziko na kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana.
- Utakuwa mwaka wa kuwafungua wanawake katika kila namna ya vifungo na umateka ili kuwaachilia kama jeshi lililotumwa na Mungu. Kina Abigaili watainuka. Kina Debora watainuka. Kina Yaeli watainuka. Hata kama walitolewa wawe mateka wa halali, mwaka huu tazamia Yaeli atamuua Sisera, Debora ataporomosha jeshi la Yabini, na Abigaili ataondoka toka katika umateka wa Nabali.
- Utakuwa ni mwaka ambao Bwana atashughulika na kila namna ya utaji wa ulaghai. Utaji wa ulaghai. Maneno ya uongo, bila kujali yamenenwa na nani na anaaminika kiasi gani, awe na joho la kisiasa, kidini, umri, mila na jadi, falsafa au joho lolote, uongo utawekwa wazi, utafichuliwa na kupata hukumu yake dhahiri.
- Mwaka huu, Mji wa Bwana, Bwana katika mlima huu atauharibu ule utaji wa sitara unaofunika fahamu za watu (Isayah 25:6-7). Watu hawatafunikwa tena! Utakuwa ni mwaka ambao Bwana atajitambulisha yeye mwenyewe kwa upya. Bwana atajitambulisha yeye mwenyewe tena kwa upya! Akisema, “Mimi Niko hapa.” Wanaomuuliza, “Bwana uko wapi?” Watamsikia akisema, “Niko hapa.” Atajitambulisha kwa sauti, atajitambulisha kwa matendo, atajitambulisha kwa mdhihirisho. Utakuwa ni mwaka ambao Bwana atajitambulisha kwa upya tena chini ya mbingu.
- Utakuwa ni mwaka wa kumwinua Modekai na kutainuka kizazi cha watu ambao hawatakuwa na michanganyo yoyote. Hakuna michanganyo yoyote! Watu wengine wakisema, “Msujudie Hamani japo kidogo ili uwe na amani,” watu hawa wamefanya maamuzi ya mioyo yao kuwa “Hakuna mungu mgeni nitakayemsujudia isipokuwa Mungu wangu mwenyewe.” Kwa kule Mungu kumuinua Modekai, Hamani kusimama hatasimama, kuanguka ataanguka kwa hakika.
- Utakuwa ni mwaka ambao kwa wale watakaodhihirisha kweli ya Mungu na kuwa na misingi ya kweli ya namna ile ya Modekai, mateso yaliyo dhahiri ya kanisa yataonekana, lakini ukombozi ndivyo unavyokuwa karibu sana. Kwa kuwa, kwa ghafla shauri la Hamani lilishindwa, na kwa ghafla Modekai alisimama.
- Utakuwa ni mwaka ambao wanaojaribu kulitesa Kanisa (mwili wa Kristo duniani) la kweli watainuka kwa nguvu. Mateso yatakuja kupitia nyanja zote. Uwanda wa kwanza unaolitesa Kanisa kwa kiwango cha juu sana ni ulimwengu wa udini. Tokea Kanisa la kwanza mpaka leo, udini ni mahala pekee ambapo Kanisa limetatanika kwa sababu limeshindwa kuelewa nafasi yake na kushindwa kuwa baraka kwa Kanisa lenyewe. Mateso ya Kanisa yatakuwa tayari kuanza, lakini mateso haya yanamaanisha ni mwanzo wa utungu kwa sababu Masihi hawezi kuruhusu Kanisa lake liteseke, atadhihirisha uwezo wake wa ukombozi. Atadhihirisha uwezo wake wa ukombozi.
- Huu ni mwaka ambao wale wanaobeba wivu wa Bwana watatembea na msaada wa malaika wa Mungu ulio dhahiri sana. Huu ni mwaka ambao wale wanaojenga watajenga kiwepesi kabisa kwa kuwa neema iliyokuwa mikononi mwa Nehemiah iko juu yao. Hakutakuwa na ugumu. Kama unajenga chochote katika huduma, katika familia, jenga wala si kidogo, ukijua ya kwamba kwa siku hamsini na mbili tu, Nehemia alijenga ukuta kuzunguka Yerusalemu yote na akaikamilisha. Huu si ujenzi wa kanuni za ujenzi, ni ujenzi kwa sababu kulikuwa na manabii waliosimama nao wakiwasaidia kuwavuvia kwa roho ya kufanya magumu yatendeke kiwepesi. “Mwaka huu na iwe Lango la kuyafanya yaliyo magumu yatendeke kiwepesi katika maisha yako.” Mwaka huu ni wakati wa matendo makuu ya Mungu. Matendo makuu na mageni kutendeka duniani. Haya ni matendo aliyosema, “Wale wamwaminio, watakuwa hodari na kutenda makuu.” Huu ni mwaka wa matendo makuu ya Mungu.
- Mwaka huu ni wakati wa matendo makuu ya Mungu. Matendo makuu na mageni kutendeka duniani. Haya ni matendo aliyosema, “Wale wamwaminio, watakuwa hodari na kutenda makuu.” Huu ni mwaka wa matendo makuu ya Mungu.
- Huu ni mwaka wa Mdhihirisho wa Lango la Masihi. Mwaka ambao Bwana anawaambia walio wake, “Tulia! Subiri uone nitakayokutendea.” Katika yale ambayo yanaonekana kuwa yanaleta taharuki kwa wanadamu, wewe utakuwa na pumziko, utakuwa na utulivu na majawabu ya Mungu yatakupa kumtukuza yeye.
- Huu ni mwaka ambao wale wenye kiu ya kumwabudu Mungu inaenda kuwapa yale ya kilindini na ushirika wa kina mahala pa Mungu kuliko nyakati zozote walizowahi kumjua. Kwa kuwa Masihi anapokuwapo, haihitaji chochote kwa mwanadamu zaidi ya kuabudiwa. Utoshelevu wao utakuja katika ushirika wa kina mbele za Mungu.
- Huu ni mwaka ambao Mungu atawapa wana wa Ufalme kuutangaza wema wake. Maana baraka itakuzunguka katika kiwango ambacho kila jicho linalokuona litasema, “Huyu amebarikiwa! Huyu amebarikiwa! Huyu amebarikiwa!”
- Huu ni mwaka ambao kutakuwa na mawimbi ya tofauti sana ya Mungu kutokea madhabahuni pake. Maana:
Nimeona ule moto unaosimama nyuma ya hao watumishi wa Mungu na ndani ya muda si mrefu nikaona miguu yangu ikivutwa kwenda kwenye hii damu inayokwenda kwa mawimbi ikitengeneza njia. Nikaona nasimama katikati yao na kwa sababu walikuwa wakienda kwa nguvu kama nguvu ya farasi, nikawa na mashaka kama ninaweza kusimama katika mawimbi ya nguvu ya namna ile. Niliposimama katika mawimbi ya nguvu ya namna ile, nikatambua kuwa nguvu ile haikuwa nguvu yao bali nguvu inayotokea ndani ya Damu ya Yesu. Kutoka saa ile nikajua ya kwamba: haya ni mawimbi yanayongoja moyo wa mtu ulio tayari—yatamchota. Haya ni mawimbi yanayotembea yenye nguvu ya tofauti sana yatokayo kwa Bwana kwa ajili ya walio wake.
"Ingia katika mawimbi haya, katika jina la Yesu. Ingia katika mawimbi haya, katika jina la Yesu!"
- Huu ni mwaka ambao Mungu atakupatia kina cha mafunuo ya kumjua yeye vya pekee. Utamjua Mungu, yeye na njia zake vya pekee! Utakuwa ni mwaka utakaoachilia moto wa utakaso. Huu ni moto unaoenda kuligusa na kulitikisa Kanisa kila kona. Kila aina ya makapi yatakaa kando, na kila namna ya agenda ya Mungu itachukua nafasi. Utakuwa ni mwaka wenye majawabu ya haraka na ya ghafla ya maombi ya watu.
- Utakuwa ni mwaka ambao utazaa matunda ya faida iliyo nyingi. Utakuwa ni mwaka ambao kila mzigo unaoelemea umeangushwa toka mabegani mwako, hautakuwa juu yako tena. Hii ni kazi ya Masihi. Utakuwa ni mwaka ambao Mungu ataiachilia neema zaidi kwa ajili ya wewe kumtii na kumtumikia Bwana Mungu wako.
- Utakuwa ni mwaka ambao Mungu atakufungamanisha na mtandao wa watu walio sahihi ambao utii umeamuriwa kwao. Huu utii si jambo la wao kuombwa bali sauti iliyoamuriwa toka kwa Mungu. Hawahitaji kushauriwa ili watii. Hawahitaji kuombwa ombwa ili watii. Utii huu ni amri, kama Daudi kwa Mungu wake.
- Huu ni mwaka ambao utele utaachiliwa kwa wale ambao ni mawakili waaminifu wa Mungu. Mungu ataachilia hazina kwa sababu umekuwa wakili mwaminifu kwa Mungu. Mungu ataachilia utele katika maisha yako na uwakili wako ukafanye vyema.
- Huu ni mwaka ambao Mungu atalipatia Kanisa mishale ya kiunabii, kama mshale wa mfalme wa Israeli ulioshikwa na Elisha (2 Wafalme 13:14–20). Ni mishale ya kiunabii ambayo mataifa yataisikia sauti ya Mungu, na ngome za uovu zitaporomoka. “Itaachiliwa juu yako Mji wa Bwana. Itaachiliwa juu yako Mji wa Bwana! Mshale wa kiunabii unaoleta majawabu kwa ajili ya taifa uachiliwe juu yako.”
- Huu ni mwaka ambao kweli inapasa kutawala. Uipende kweli. Nawe uipende zaidi ya kuwekea mashaka katika eneo lolote. Huu ni mwaka ambao Bwana ataachilia mabadiliko endelevu ambayo yataachiliwa katika maisha yako kupitia uwepo wake. Huu ni mwaka ambao unyenyekevu na moyo uliopondeka utavutia uwepo wa Mungu, na malaika wa Mungu walio wangojezi wataambatana na maisha yako. Kabla hujasema chochote, unyenyekevu wako na moyo uliopondeka utafanya malaika wa Mungu waambatane na maisha yako kwa agenda ya msaada wa Mungu.
- Huu ni mwaka ambao Mungu atawapatia wengi habari iliyo njema, iliyongojewa kwa muda mrefu. Habari iliyo njema! Kwa kuwa Mdhihirisho wa Lango la Masihi ni habari njema ya agenda ya ghafla ya Mungu, matendo ya ghafla yatamtambulisha Masihi katika maisha yako. Huu ni mwaka ambao Mungu atamhukumu Hamani, “Hamani” yeyote katika maisha yako. Kwa kuwa Masihi hawezi kushindania kiti na Hamani.
- Hatimaye, huu ni mwaka wa mapambano kwa vita ya maneno. Bwana ataweka upanga mkali kinywani mwako. Wao watakuwa na maneno lakini maneno yako yatakuwa upanga. Wao watakuwa na maneno lakini maneno yako yatakuwa upanga! Tumia vema kinywa chako! Tumia vema kinywa chako! Upanga hautumiwi kila mahala, upanga unafanya kazi yake mahala sahihi. Mungu anapofanya kinywa chako kuwa upanga, jua namna ya kuweka alani upanga wako.
"Mwaka huu Mungu atawapatia wengi habari iliyo njema, iliyongojewa kwa muda mrefu."
Mji wa Bwana
Wewe ni kama ule mji mdogo wa Bethlehemu. Bwana anasema nyota yako imeonekana katika mataifa ya mbali, na hivyo, mataifa yameachilia hazina yake ili kukutumikia. Yeye akulindae atatetea mashauri yote aliyoweka ndani yako.
Ameamuru nyakati za kukamilishwa kwa mambo yako yote ili upate kuwa mahala pa kimbilio kwa walio wengi. Anasema, “Nimekupa neema na kibali ili upate kudhihirisha nguvu yangu na utukufu wangu katika mataifa na katikati ya miaka. Kudhihirisha nguvu yangu na utukufu wangu katika mataifa na katikati ya miaka! Nimeukemea udhaifu, nimekemea kila hali ya kwenda kwa uzito, iondoke miongoni mwenu. Iondoke miongoni mwenu! Kwa kuwa wote wanaoamini kwamba nimewainua kwa ajili ya yale yaliyo makuu usoni pa nchi, yaliyo makuu yatakuja katika maisha yao bila mahangaiko. Bila mahangaiko! Bila mahangaiko!”
Na hapa, Bwana akanena maonyo kwa namna ya maono yaliyo kielelezo. Akasema:
Uwe mwangalifu. Wanaoikosa nuru ya nyota ile ya Bethlehemu, wanapitwa na malango ambayo yanaweza kuwapa machozi na yanaweza kuwapa hasara. Nyota ilionekana mataifa ya mbali, lakini wa Bethlehemu hawakuwa na habari ya nyota hiyo wala kilichoendelea. Waliotoka mataifa ya mbali waliabudu na Yesu aliondolewa toka Bethlehemu, na walioko Bethlehemu watoto wao wote, miaka miwili kushuka chini, waliuawa kwa sababu Masihi amekuja kwao. Masihi hakuuawa, lakini wao ndio waliopata hasara. Lango hili la Masihi juu yako Mji wa Bwana, nyota yako imeonekana tokea mbali! Simama vema katika malango ya walinzi ili wale Mungu aliokupa dhamana kuwaponya wasiuawe kwa ajili yako, wasipotee kwa ajili yako.
ENCC
Fungua macho yako utazame, weka moyo wako kuitafuta hekima. Kwa kuwa nitauondolea mbali udhaifu wako wote na kukuponya jeraha zako. Nasimama nikiwa na fimbo yangu ya mamlaka kwa ajili yako. Kama ukiwa tayari, ukiwa una utashi, ukikubali na kutii, nitakutia nguvu na kuundolea mbali udhaifu wako.
Na hapa tena hii ilikuwa ndiyo sababu ya mimi kumuona Masihi akiwa na fimbo, na fimbo hii aliita Fimbo ya Mamlaka yake. Haishiki Fimbo hii ya enzi kwa ajili yake mbinguni, hii ndio Fimbo aliyosema, “Tawala wewe kati ya wakuchukiao mpaka nitakaporejea.”
Fimbo hii inaachiliwa juu yako ili kusudi udhaifu ulionao uondoke. Ufunguo wake: weka moyo wako katika kuitafuta hekima na moyo wa ufahamu.
Tanzania
Tanzania, tatizo lako ndilo tatizo la Afrika. Tanzania, tatizo lako ndilo tatizo la Afrika! Nchi yako imejeruhiwa. Nchi yako imeharibiwa na misingi ya kiti chako cha enzi imenajisiwa kwa damu. Misingi ya kiti chako cha enzi imenajisiwa kwa damu! Je, huwezi kusikia sauti ya damu?
Je, huwezi kusikia sauti ya mlipiza kisasi cha damu? Kwa kuwa kiti chako cha enzi kimenajisiwa kwa damu, naiita Tanzania kwenda magotini kwa toba ya kweli. Toba yenye kubadilisha mioyo wala si toba ya maneno matupu. Toba ya watu wanaoona hatia yao mbele za Mungu wala si kujitafakari mbele ya wanadamu. Kwa kuwa kabla misingi ya haki haijapinduliwa, Lango la Masihi lapasa kupindua misingi ya udhalimu, misingi ya uovu, ili misingi ya haki ipate kusimama tena. Kwani wewe hukujua ya kwamba jina la Masihi humaanisha ‘Yeye atawalaye kwa haki.’ Humaanisha ‘Haki iliyo ya Mungu imedhihirika ndani ya mwanadamu.’
Huu sio wakati wa kunyoosha kidole kwa mwingine. Hakuna asiyekubali kwamba tumejeruhika hivyo si wakati wa kusema ‘Ni kwa ajili yako, au kwa ajili ya yule,’ haitamsaidia awaye yote. Ni wakati wa makuhani wamchao Bwana kusimama mahala pa Madhabahu ili walilete Taifa magotini mbele za Mungu na watu waseme kwa Mungu, “Zawadi ya uhai ulio tupatia, tumeichezea.”
"Na kwa sura hiyo, 2026 kuna Mdhihirisho wa Lango la Masihi. Masihi mwenyewe ni jambo jingine tofauti, na Lango lake kutenda kazi ni jambo jingine tofauti. Yeye hana mwingiliano wowote na kiumbe yoyote, lakini wewe utakuwa Lango la Masihi."
